Advertisements

Tuesday, April 11, 2017

Diamond alivyozua mjadala, wimbo wake wachambuliwa



Msanii Diamond Platnumz
By Ras Inno Nganyagwa

Mjadala unaofukuta kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wimbo mpya wa msanii Diamond Platnumz umewagubika waliokuwamo na wasiokuwamo, kwani licha ya mashabiki wa muziki lakini hata wasioshabikia nao wamejitosa kutokana na ‘tafsida tata’ iliyofichwa kwenye mashairi aliyoimba.

Na ingawa ni rahisi kuelewa nini kilicholengwa kutokana na hamkani za matukio ya hivi karibuni yanayosababisha siasa na muziki kuteka akili za Watanzania wengi. Kabla sijazama katika wimbo wenyewe ni vyema kukumbushana kwamba huo si wimbo wa kwanza kusababisha utata.

Baadhi ya nyimbo zilizowahi kusababisha mtafaruki wa tafsida ni: ‘Bunduki Bila Risasi’ wa Hayati Bi Shakila uliowahi kuharamishwa kuchezwa hewani, nyingine ni pamoja na wimbo wa Mgunga Mwamnyenyelwa wa maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, kutokana na mashairi yaliyotafsiriwa kinyume na fasihi aliyomaanisha.

Lakini hivi karibuni Ney Wa Mitego aliwekwa rumande na kutoka kwa amri ya Rais John Magufuli aliyebainisha kuvutiwa na Ney kuelezea yanayoizunguka jamii yetu kwa sasa, lakini Roma Mkatoliki ambaye naye alikumbwa na masaibu ya kutekwa na kuibuka anafahamika kwa nyimbo zenye maneno makali ambazo hazipigwi kwenye vituo vya redio na runinga, lakini ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya usafiri zikiwamo bodaboda. Ili kupata kina cha uhakiki wa wimbo wa Diamond (Nikae Kimya) kutokana na mvutano ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii, nililazimika kuutafuta na kuusikiliza kwa kina na kubaini mambo kadhaa. Kwanza anaeleza kujizuia kwake kuingia kwenye fukuto la mijadala inayoendelea kutokana na matukio ya sasa hapa nchini, lakini pia ustahimilivu ulivyomshinda kutokana na kusakamwa kwa kimya chake akihisiwa ni muoga kutokana na ulemezi wake kwa baadhi ya wanaosemwa, akaeleza hisia za kushindwa kusambaza wimbo wa rafiki yake ambaye alisikitika alivyowekwa rumande.

Mwanzoni anataja anayechochea mitandaoni yanayoendelea lakini mwishoni akitaka hayo yote yaachwe ili watu wazingatie mambo muhimu, ikiwamo kufanya kazi na kutotekwa na hisia za kisiasa zilizoingia kwenye wigo wa muziki. Ukweli wa mirindimo ya wimbo unajibainisha kwani ni wimbo wenye masononeko na haujiakisi kujaa kedi ya kutetea upande wowote, kwa kuwa katika weledi wa muziki mashairi yanayowasilishwa hubebwa na mikong’osio inayoshadadia uzito wa ujumbe kama alivyofanya Ney katika ‘Wapo’ au nyimbo nyingi za Roma Mkatoliki.

Sehemu ya pili ya kinachobainishwa katika wimbo huo ni kuisema mamlaka kwa ukimya wa yanayotokea yanayokengeusha fikra za watu badala ya kuzingatia mambo ya kimsingi.

Ni ukweli kuwa matukio ya ‘kiki’ za kisiasa zinazotoshana nguvu na muziki yanatawala kwenye mijadala na kula muda mwingi wa mambo mengine, ingawa ni faraja kwa waliokosa la kufanya ambao wamepata cha kujishughulisha nacho.

Lakini athari zinazoibua hamkani ya shutuma kama Diamond kwa kutoa wimbo huo amepatia au amekosea ni matukio yasiyofaa yanayoendelea nchini kwa siasa kuuteka muziki na kusababisha mgawanyiko wa mtazamo, ingawa kwa uyakinifu tafsida zinazoimbwa kwenye nyimbo zina maana halisi ya fasihi aliyodhamiria kuiwasilisha mtunzi si makisio ya mashabiki kutokana na mtazamo wa fikra zao.

‘Nikae Kimya’ imegusa kada mbalimbali bila uelemeo wowote, mamlaka, wananchi wanaoshabikia kiki za matukio yanayojiri, watu maarufu wa kada mbalimbali na hata wasanii. Siasa na muziki ni ndugu wanaoshadadiana kwa upatano wa heri na wakati mwingine hamkani za shwari!

0628 011 223

No comments: