Advertisements

Thursday, June 6, 2024

WAKUU WA TAASISI ZA USAFIRI WA ANGA - AFRIKA WAKUTANA JIJINI ARUSHA

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akipokea hati ya shukrani kutoka kwa Rais wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC) Bw. Silas Udahemuka ikiwa ni ishara ya kuipongeza na kuishukuru Tanzania kwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa pili wa Kamisheni unaowakutanisha Wakurugenzi Wakuu wa taasisi za Usafiri wa Anga Afrika unaofanyika kwa siku mbili jijini Arusha kuanzia tarehe 5 Juni 2024. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisoma hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC)

Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC) Bi. Adefunke Adeyemi akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC)
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC)
Rais wa Kamisheni ya Usafiri wa Anga Afrika (AFCAC) Bw. Silas Udahemuka akiteta jambo na Mtendaji Mkuu wa AFCAC Bi. Adefunke Adeyemi wakati wa ufunguzi wa mkutano wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TCAA, Dkt. Khamis Mwinnyimvua
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akiongea na wanahabari mara baada ya kufungua mkutano
Picha ya pamoja

Wakuu wa taasisi za Usafiri wa Anga Afrika wanakutana jijini Arusha, Tanzania kujadili kwa Pamoja namna bora ya kuboresha sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika.

Akizungumza wakati wa kuufungua mkutano huo,Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika imekuwa ikipiga hatua kusonga mbele lakini juhudi za Pamoja zinahitajika ili kuongeza kasi ya ukuaji wake.

Prof. Mbarawa amesema mkutano huu ni muhimu sana na unafanyika wakati sahihi ambapo uelewa wa wananchi wengi juu ya Usafiri wa anga umeongezeka.

"Ni heshima kwetu kama nchi kupata fursa ya kuandaa mkutano huu, sina shaka kuwa mtajadili na kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya bara letu la Afrika" amesema Prof. Mbarawa

Kwa upande wa Rais wa Kamisheni hiyo Bw. Silas Udahemuka ameishukuru Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji na kuandaa mkutano huu na kuwataka wajumbe kuitumia vyema fursa hii kupanga na kujadili mambo chanya yatakayoleta utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hii barani Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Bw. Hamza Johari amesema mkutano huu siyo tu unawakutanisha wakuu wa taasisi kujadili utatuzi wa changamoto bali ni kuwa na sauti ya Pamoja kama Afrika katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha maslahi ya Afrika yanazingatiwa.

Mkutano huu wa pili unafanyika kwa siku mbili katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha na wajumbe watapata nafasi ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii nchini.

No comments: