Advertisements

Thursday, June 13, 2024

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO KWA WATUMISHI WA UMMA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini kote wawatumikie wananchi ipasavyo na wahakikishe wanaondoa urasimu kwa kutowasumbua wananchi wanaokuja kupata huduma za kiserikali katika ofisi zao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaa Tanzania (TOA) unaofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha.

“Epukeni tabia ya kuomba na kupokea rushwa, rushwa inaharibu maendeleo. Tusitumie maneno magumu kwa wananchi wetu maana eneo hili bado ni changamoto, tunalishughulikia au bado tupo kwenye mchakato, tunafanya tathmini, upembuzi yakinifu, tumieni lugha rahisi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie taaluma zao na watoe ushauri kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, wafike sehemu ya kazi kwa muda uliopangwa na watumie muda huo kufanya kazi za Serikali na waepuke kuwa na migongano ya maslahi katika kutekeleza majukumu na kusimamia rasilimali za umma.

“Viongozi wote tuwahudumie wananchi kwa heshima, staha, unyenyekevu na umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwapa majibu sahihi ya maswali yao na majawabu sahihi ya kero zinazowasumbua. Toeni ufafanuzi au maelekezo juu ya masuala yatokanayo na sheria, kanuni na taratibu za Serikali kwa haraka, uwazi na bila upendeleo wowote au ubaguzi wa aina yoyote.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha wananchi wote wanapata maendeleo na huduma mbalimbali za msingi.

Amesema chombo muhimu cha kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wa ngazi ya msingi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa na maendeleo hayo yatakuwa dhahiri na endelevu endapo wananchi watashirikishwa katika kuainisha changamoto zinazowakabili na watawezeshwa kukabiliana nazo kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.


Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanakuwa na mifumo madhubuti ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato pamoja na kuweka mkakati wa udhibiti wa mali zilizopo ndani ya halmashauri na mapato watakayoyapata wayaelekeze katika kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri zao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema wizara yao itaendelea kufanya maboresho ya utendaji kwa watumishi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Akizungumzia kuhusu TOA, Dkt. Dugange amesema taasisi hiyo imesaidia kuboresha utendaji wa watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa kupitia mafunzo yanayotolewa ambayo yamekuwa na tija kwa Taifa kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato kupitia ushuru, ada na tozo mbalimbali.

Awali, Mwenyekiti wa TOA Taifa, Bw. Albert Msovela alisema lengo kuu la taasisi hiyo ni pamoja na kuchangia kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala yote yanayohusiana na fedha, utawala na utoaji wa huduma katika misingi ya ugatuzi wa madaraka (Decentralisation by Devolution – D by D) na kutetea dhana ya ugatuaji wa madaraka katika ngazi zote za Serikali.

Mwenyekiti huyo alisema lengo lingine ni kuwaleta pamoja wadau wote wa Serikali na sekta binafsi ili kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa dhana ya ugatuzi wa madaraka katika maboresho ya Serikali za mitaa nchini pamoja na kukuza uwekezaji katika ngazi za msingi (Local Economic Development - LED).

Akizungumzia kuhusu mafanikio ya TOA, Bw. Msovela alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa fedha za maendeleo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi za msingi, kuwepo kwa mifumo ya kusimamia matumizi ya fedha za Serikali.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na upangaji mipango katika Halmashauri na kuanzishwa kwa mfumo wa Ruzuku ya Maendeleo kwa Serikali za Mitaa (Capital Development Grant - CDG) kama sehemu ya ugatuzi wa masuala ya kifedha. “Fedha kutoka mfuko huu zilisaidia sana katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye jitihada za wananchi.”




No comments: