Wednesday, October 9, 2024

WAKATI UMEFIKA WA KUREJESHA DIPLOMASIA YA UCHUMI NA KUENDELEZA BIASHARA BAINA YA ZANZIBAR NA COMORO


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Gavana wa jiji la Moroni, Comoro Mhe Ibrahim Mzee (kulia kwa Rais) akiongoza ujumbe huo, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 9-10-2024, na (kushoto kwa Rais) Mstahiki Meya wa Jijini la Zanzibar Mhe. Mhamoud Muhammrd Mussa.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Gavana wa jiji la Moroni, Comoro Mhe Ibrahim Mzee (kulia kwa Rais) mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 9-10-2024
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na mgeni wake Gavana wa jiji la Moroni, Comoro Mhe Ibrahim Mzee, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 9-10-2024.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wakati umefika wakurejesha diplomasia ya Uchumi na kuendeleza biashara baina ya Zanzibar na Comoro kwa maslahi ya pande zote mbili.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo, Ikulu Zanzibar alipozungumza na Gavana wa jiji la Moroni, Visiwa vya Ngazija, Bw. Ibrahim Mzee aliefika na ujumbe wake kuwasilisha dhamira ya kukuza ushirikiano baina nchi mbili hizo.

Rais Dk. Mwinyi aliushauri ujumbe huo kurejesha makundi ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja Zanzibar kuangalia fursa za biashara na uwekezaji kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Amesema, ni vyema kwa pande mbili hizo kufirikia namna ya kurejesha huduma ya usafiri wa vyombo vya baharini ili kuwanufaisha wananchi wa pande mbili hizo na fursa za biasahara na kijamii ziliopo.

Aidha, Dk. Mwinyi alishauri ujumbe huo kuweka utaratibu maalumu kwa walimu wa Zanzibar kwenda Comoro kufundisha Kiswahili au Wakomoro kuja Zanzibar kujifunza lugha hiyo jambo ambalo alisema litakuwa na wepesi kwani lugha za nchini mbili hizi zinashabihiana.

Naye, Gavana Ibrahimu Mzee amesifu kasi ya mabadiliko na maendeleo makubwa ya Zanzibar na kusema kuwa nchi yake inakitu cha kujinza kama ilivyofanikiwa ya Zanzibar.

Alitumia fursa hiyo, kumualika Rais Dk. Mwinyi kuzuru visiwa vya Ngazija kwalengo la kubadilishana uzoefu kwenye nyanja za maendeleo.

Eneo jengine alililoligusia ni kuimarisha ushirikiano wa karibu baina ya Jumuiya ya Wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda (Chamber of commerce) ya Zanzibar na ile Comoro ili kukuza biashara.

Akiambatana na ujumbe huo Meya wa jiji la Zanzibar, Mahmoud Muhammed Mussa ameelezea ujumbe wa Gavana huo utakuwepo Zanzibar kwa siku tatu na kueleza kuwa na mazungumzo ya ushirikiano baina ya Manispaa ya jiji la Zanzibar na Manispaa ya jiji la Moroni.

Aidha, ujumbe huo utakuwa na siku maalum ya kuutembelea mji Mkongwe wa Zanzibar ambao mji wa urithi uanaotambulika na UNESCO. Pia ujumbe huo utafanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa kwa lengo la kukuza ushirikiano.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments: