Advertisements

Tuesday, December 1, 2015

Kampuni D’ salaam yatengeneza miguu bandia kwa majaribio


By Bakari Kiango, Mwananchi

Dar es Salaam. Kampuni ya Kamal Group ya inayojihusisha na utengenezaji wa nondo, imetengeneza miguu bandia ya majaribio na kuigawa kwa watu 60 wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Satyam Gupta alisema jana kuwa wana wajibu wa kusaidia maendeleo ya jamii ndiyo maana wamefanya majaribio hayo.

“Ni wajibu wetu kuleta tabasamu katika nyuso za watu wanaotuzunguka na kuhakikisha kuwa wale wenye ulemavu wa miguu wanaweza kutembea,” alisema Gupta.

Gupta alisema miguu hiyo imetengenezwa na wataalamu kutoka India kwa kutumia mitambo ya kiwanda hicho.

“Nia yetu ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanarudi katika sehemu zao za kazi ili watoe michango yao katika kuijenga Tanzania, kwa vile tuna kiwanda chenye zana za kimataifa nchini. Tulilazimika kuwaleta wataalam ili kazi yote waifanyie hapa nchini. Tulichoagiza hapa kutoka nje ya nchi ni malighafi tu,” alisema Gupta.


Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), John Mlabu alisema bei ya mguu mmoja bandia kwa sasa inafikia Sh4 milioni, hivyo wengi wao kushindwa kumudu kununua.

“Tunaishukuru sana kampuni ya Kamal kwa msaada huu wa kugawa vifaa kwa mikoa ya Arusha na Mwanza na tunaomba kampuni nyingine ziige,” alisema.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni mbili wenye uhitaji wa viungo bandia, lakini kutokana na gharama kuwa kubwa, ni asilimia 20 tu ndiyo wenye uwezo wa kununua.

Kampuni hiyo pia inaendesha mradi wa chakula kwa wanafunzi 1,250 kila siku kwa shule za msingi za Nzasa ya Ilala jijini Dar es Salaam na Kerege ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mradi huo ulioanza kitekelezwa mwaka jana, utarajia kuwafikia wanafunzi 3,000 ifikapo mwaka 2017.

No comments: