JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA
MAKAMU WA RAIS
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU ZOEZI LA KUHAMISHA WAKAZI
WA MABONDENI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Utangulizi
Nchi yetu ina kingo za
mito na mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume cha
sheria, huku wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao. Kutokana na uhaba wa makazi, hali ni mbaya
zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde la Mto Msimbazi.
Serikali za awamu
zote, zimekuwa zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni
wanaoishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya
kuridhisha.
Serikali ya Awamu ya
Tano, ambayo moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza
jitihada za kuwaondoa wakazi hawa. Tuliamua kuanza na Bonde la Mto Msimbazi
kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari kubwa.Sababu zetu kuu za
kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na
mazingira yanayozunguka ni:-
- Kunusuru maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.
- Kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua nyingi;
- Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu, hasa wakati wa mvua;
- Kuzuia eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho ya wahalifu na uhalifu;
- Kutoa nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu wa Zoezi
Kabla ya nyumba
kubomolewa, taasisi hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi
ina nyaraka za umiliki na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali
wowote. Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo katika maeneo yasiyostahili ndio
zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya
hapo, mkazi hupewa muda wa kubomoa na kuhama mwenyewe.
Kutokana na utaratibu
huu, sehemu kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua
kubomoa wenyewe. Baada ya hapo, alama huwekwa kuonyesha mpaka wa bonde. Katika
zoezi hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya wakazi wa maeneo ya mabondeni ni
wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu nyingine salama. Serikali pia imeweka
Dawati la Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini
ya Zoezi
Jana, terehe 7 Januari 2016, Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), walifanya mkutano wa
kutathmini zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano huo ulipokea ripoti ya timu ya wataalam wa Wizara mbalimbali,
inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambayo,
pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba sehemu kubwa ya kubaini makazi
yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la Mto Msimbazi imekamilika.
Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa, wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa
pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa
kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa makazi anayoishi hufanywa. Kutokana na
uhakiki huo, jumla ya wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119
walikuwa na leseni za makazi za muda mfupi. Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri
walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi
hilo. Baada ya tafakuri na mjadala, Mawaziri
hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa Serikali: -
1. Zoezi la kuwaondoa wananchi waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo
hatarishi) litaendelea kwa utaratibu ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa
wananchi;
2. Katika awamu hii, zoezi litajikita katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3. Kwa wakati huu, watakaohitajika kuhama ni wale tu ambao makazi yao
yamo NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na kwenye KINGO
za mto;
4. Wale watakaokuwa na nyaraka halali walizopewa na mamlaka za umma,
zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika bonde hilo, hawatahamishwa bila
kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi wa umma waliowamilikisha maeneo
hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria;
5. Serikali, ndani ya siku tatu zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi
na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji umefanyika.
6. Serikali itaheshimu amri za mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa
na baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka
ili taratibu zinazofuatia zifanyike;
7. Serikali itawachukulia hatua
za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya
sheria zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo
wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la
malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya
kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.
8. Nyumba na majengo ya miaka mingi, yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya
kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi hili, hayatabomolewa isipokuwa tu
pale maisha ya wakazi yapo hatarini. Wanaoishi katika makazi hayo watapewa
miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira na kujiokoa na maafa;
9. Serikali haina dhamira ya kubomoa mahoteli makubwa ya siku nyingi
yaliyo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki. Wamiliki wa mahoteli haya
watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria.
10. Serikali inaweka uratibu wa karibu zaidi
miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za nchi zisiwe
chanzo cha taharuki katika jamii.
11. Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha
kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi
kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa
maisha yao yapo hatarini. Itakumbukwa kwamba katika mafuriko ya mwaka 2011,
wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha. Kwa mujibu wa taarifa ya
Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha mvua kubwa kuliko
zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
12. Serikali inafuatilia kwa karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu
ya taarifa za wananchi wanaohitaji msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la Mchungaji Getrude
Rwakatare
Mkutano ulipokea taarifa kuhusu suala linaloongelewa sana la nyumba
ya Mchungaji Rwakatare. Ilielezwa kwamba
Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko wa mto
kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko, kinyume
kabisa na Sheria tatu muhimu. Pia
ilielezwa kwamba tangu wakati ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha
zilifanyika na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini ikashindikana kutokana na
sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa
mahakamani. Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa
Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe
11 Mei 2015, aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba
ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza,
kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei
2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba
2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kufuata taratibu zote, alishaagiza
kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa
zake zimekwishafikishwa TAKUKURU. Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais, iliiagiza
Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake na
Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya
udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu
hoja inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi
mabondeni lakini mradi wa DART umeachwa. Mkutano ulielezwa kwamba Sheria ya
Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa miradi/shughuli
zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni, na kwamba Waziri
mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna ya shughuli hizo
zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira. Mradi wa DART ulipata kibali
hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya
mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
1 comment:
Hii ndio Tanzania ninayoanza kuihisi itakua ile Tanzania yakila mtu kuwa kwenye mstali ! Sikubaliani na bomoabomoa bila kuwaandalia mazingila mbadala ! Ila kitendo cha viongozi kukaa chini na kutoa taarifa kama hivi , kwakweli sio siri sasa binafsi yangu naanza kuona Tofauti ya uongozi wa sasa na viongozi walio pita ! Tuna rudi kule kule kama utawala huu mnaweza na mnajiamini wekeni katiba ya Warioba muone Tanzania patakapo chimbika mwendo wa jino kwa jino ! Kinyume na hapo bado nnawasi wasi na hii spidi ! Ila kwa kitendo chakutoa taarifa kama hiyo nawapongeza sana ! Mwanzo mzuri !
Post a Comment