Rais mteule wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameapishwa kushika hatamu ya uongozi visiwani Zanzibar na kusema serikali yake italinda haki za raia, kuhimiza uwajibikaji na usawa pasipo kubagua mtu yeyote.
Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja, Rais Shein pia ameahidi kuunda serikali itakayounganisha Wazanzibar na kwamba atahakikisha misingi ya Muungano iliyowekwa wakati wa kuasisiwa kwake inadumishwa.
Dk Shein ameapishwa leo kufuatia ushindi aliopata Jumapili iliyopita wa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 ya kura zote halali 328,327 zilizopigwa katika uchaguzi marudio.
Uchaguzi huo umerudiwa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa Disemba 25, 2015 kwa kile alichodai kukithiri kwa dosari.
Katika uchaguzi wa marudio Chama Cha Wananchi (CUF) kilichoshiriki kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) muhula wa 2010-2015 hakikushiriki kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka jana.
Sherehe za leo visiwani Unguja vimehudhuriwa na viongozi wastaafu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar na viongozi wa Serikali ya Muungano waliopo madarakani akiwemo Rais John Magufuli, Makamu wake Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa Kasim Majaliwa.
No comments:
Post a Comment