Thursday, August 20, 2015

BALOZI SEIF AWAPOKEA VIJANA WALIOJIUNGA NA CCM NA KUANZISHA MASKANI KIJIJI CHA KINAZINI MTAMBWE KUSINI

Kijana Ali Abdulla Bakari wa Balozi Seif Maskani ya kijiji cha Kinazini Mtambwe Kusini akieleza changamoto zinazowakabili wakati Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif alipofanya ziara ya kuwatembelea baada ya uamuzi wao wa kujiunga na CCM na kuachana na upinzani.
Balozi Seif akizungumza na Wana CCM na wanamaskani wa Balozi Seif wa Kinazini Mtambwe na kuahidi kwamba CCM inasaidia ujenzi wa Jengo la Maskani yao waliyoianzisha.
Balozi Seif akimkabidhi mchango wa shilingi Milioni 1,000,000/- Katibu wa Maskani ya Balozi Seif ya Kijiji cha Kinazini Mtambwe ili kuanzia msingi wa Jengo lao la Maskani.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa CCM Balozi Seif akibadilishana mawazo na Vijana wa Maskani ya Maida Mtambwe baada ya kuwasalimia kwa muda mfupi alipokuwa katika ziara ya Mkoa Kaskazini Pemba. Picha na –OMPR – ZNZ. 


     Na Othman Khamis Ame, OMPR 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Chama hicho kiko makini katika kumuengua Mwanachama wake yeyote anayetumia hila katika mchakato wa kutaka achaguliwe kuwa Kiongozi kupitia chama hicho. 

Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza na Vijana walioamua kutoka chama cha Upinzani na kujiunga na CCM ambapo wameanzisha Maskani iliyopewa jina la Balozi Seif Maskani hapo katika Kijiji cha Kinazini Mtambwe Kusini. 

Balozi Seif ambae alipata wasaa wa kuikagua Maskani hiyo na kuahidi kusaidia ujenzi utakaolingana na hadhi ya Chama chenyewe alisema CCM kuendelea kukumbatia wala rushwa ni sawa na kwenda kinyume na Sera na Ilani yake. 

Alisema maamuzi yaliyofanywa katika vikao mbali mbali vya Viongozi wa ngazi za juu ya Chama hicho kuwaengua wanachama waliotumia njia ya rushwa katika kusaka Uongozi yalikuwa sahihi na yanapaswa kuungwa mkono na Wanachama pamoja na wapenda haki wote Nchini. 

Aliwatoa hofu wana CCM na Wananchi wote kwamba Chama cha Mapinduzi kimekuwa na utaratibu wa kuhusisha wanachama wake katika mchakato wa kuchaguwa Viongozi wake kwa kutumia mfumo wa Demokrasiaya wengi iliyokomaa. 

Balozi Seif amewapongeza Vijana hao wa Kijiji cha Kinazini Mtambwe Kusini kwa uamuzi wao wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi chenye Sera na Ilani inayotekelezeka. 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwaahidi Vijana hao kwamba CCM itawapa neema kwa kuwasimamia kutatua changamoto zinazowakabili katika harakati zao za kujitafutia maendeleo. 

Balozi Seif Ali Iddi aliwaonya Viongozi na wanachama wa upinzani kusitisha tabia ya kumzushia pamoja na kumsakama bila ya sababu za msingi kwa mambo ambayo hajayafanya. 

Mapema akisoma risala Mmoja wa Vijana wa maskani hiyo ya Balozi Seif Ndugu Ali Abdulla Bakari alisema uamuzi wao umefuatia vijana hao kukosa maendeleo waliyokuwa wakiahidiwa na Viongozi wa upinzani kwa zaidi ya miaka 20 sasa.





Nd. Ali alisema kundi kubwa la Vijana walioko ndani ya Kijiji hicho na vile vya jirani wamekosa kupatiwa huduma muhimu zikiwemo mitaji ya kuendesha miradi yao ambayo ingewasaidia katika kujikwamua na wimbi la ukali wa maisha. 


Alisema Vijana wengi wa maeneo hayo ambao wana taaluma ya miradi ya uvuvi wameshindwa kuimarisha miradi hiyo kwa kukosa vifaa vya kuvulia kama boti pamoja na zana zake. 


Kijana huyo wa Makasni ya Balozi Seif Kinazini Mtambwe Kusini kwa niaba ya wenzake wamewaomba viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi za Jimbo, Wilaya na Mkoa kuendelea kuwapatia darasa la itikadi kwa lengo la kuelewa Sera na Ilani ya Chama chao walichoamuwa kukitumikia hivi sasa. 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa pia alipata fursa ya kusalimiana na Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Maskani ya Maida iliyopo Mtambwe na kubadilishana nao mawazo kwa muda mfupi. 

Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi kamwe hakidharau Wanachama wake popote pale walipo hata kama atakuwepo mmoja na ndio maana yeye anakuwa tayari kumtembelea na kutaka kujuwa changamoto zinazomkabili.

No comments: